Dhikri bora zaidi: SubhanAllah, Alhamdulillah, La ilaha illallah

Maneno mafupi ya dhikri yenye malipo makubwa, kwa wakati wowote wa siku.

1 Mara moja

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ

Maana na chanzo

Imepokelewa Kutoka kwa Jabiri -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani ziwe juu yake- akisema: "Dhikiri bora ni: Laa ilaaha Illa llaah: Na dua bora ni: Al-hamdulillah".

Imepokelewa na Tirmidhiy na Nasai katika kitabu Alkubraa na Ibn Majah Daraja: Ni nzuri (Hasan)

Maelezo

Anatueleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa dhikiri bora ni: "Laa ilaaha illa llaah" Na maana yake, hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa dua bora ni "Al-hamdulillaah"; Nayo inamaanisha kukiri kuwa mneemeshaji ni Mwenyezi Mungu -Aliyetakasika na kutukuka-, mwenye kustahiki sifa nzuri zilizokamilika.

Faida

  • Himizo la kukithirisha kumtaja Allah kwa neno la tauhidi (Laa ilaaha illa llaah), na kuomba kupitia himidi (Shukurani kwa Allah).

Soma kwenye HadeethEnc.com

2 Mara moja

سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ

Maana na chanzo

Imepokewa kutoka kwa Jundubi -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- "Maneno yanayopendeka zaidi kwa Allah ni manne: Sub-haanallah, Al-hamdulillaah, na Laa ilaaha illa llaah, na Allahu Akbar, haidhuru ikiwa utaanza na lolote kati ya hao".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Anabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa maneno yanayopendeka zaidi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni manne.

Sub-haanallaah: Na hili linamaanisha kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila aina ya mapungufu.

Na Al-hamdulillaah: Nako ni kumsifu Allah kwa ukamilifu uliotimia pamoja na kumpenda na kumtukuza.

Na Laa ilaaha illa llaah: Yaani: Hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Allah.

Na Allahu Akbaru: Yaani: Ni Mtukufu mno, na ni Mtakatifu mno kuliko kila kitu.

Nakuwa fadhila zake na kupata thawabu zake si lazima kuyapangilia wakati wa kuyatamka.

Faida

  • Wepesi wa sheria, kiasi kwamba haidhuru kwa neno lipi kati ya hayo utaanza nalo.

Soma kwenye HadeethEnc.com

3 Mara moja

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ

Maana na chanzo

Imepokewa Kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Maneno mawili mepesi mno katika ulimi, ni mazito mno katika mizani, yanapendeka mno kwa Al-Rahmani (Mwingi wa rehema) Ni: Sub-haanallahil Adhwiim, Sub-haanallaahi wabihamdihi".

Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake Daraja: Sahihi

Maelezo

Ameeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-kuhusu maneno mawili anayoyatamka mwanadamu bila uzito wowote na kwa hali yoyote, nakuwa maneno hayo malipo yake ni makubwa katika mizani, nakuwa Mola wetu Mlezi Mwingi wa rehema -Aliyetakasika na kutukuka- anayapenda:

Sub-haanallahil Adhwiim, Sub-haanallahi wabihamdihi; Kwakuwa yamekusanya sifa miongoni mwa sifa za Allah kumsifu kwa Utukufu na ukamilifu, na kumtakasa kutokana na mapungufu -Aliyetakasika na kutukuka-.

Faida

  • Dhikri tukufu zaidi ni ile inayokusanya kati ya kumtakasa Allah pamoja na kumtukuza.
  • Kumebainishwa upana wa rehama ya Allah kwa waja wake, kwani Yeye analipa kwa amali ndogo thawabu nyingi.

Soma kwenye HadeethEnc.com

4 Mara moja

سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ

Maana na chanzo

Imepokewa kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Kusema kwangu: Sub-haanallaah, na Alhamdulillaah, na Laa ilaaha illa llaah, na Allaahu Akbaru, kunapendeka sana kwangu kuliko vitu vyote vilizochomozewa na jua".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Anaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa kumtaja Allah Mtukufu kwa maneno haya matukufu ni bora kuliko dunia na vilivyomo, na utajo huo ni kusema:

"Sub-haana llaah": Ni kumtakasa Mwenyezi Mungu kutokana na mapungufu.

"Alhamdulillaah": Ni kumsifia kwa sifa za ukamilifu pamoja na kumpenda na kumtukuza.

"Laa ilaaha illa llaah": Hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.

"Allaahu Akbaru: Mkubwa na Mtukufu kuliko kila kitu.

Faida

  • Himizo la kumtaja Mwenyezi Mungu, nakuwa hilo linapendeka zaidi kuliko vyote vilivyochomozewa na jua.
  • Himizo la kukithirisha dhikiri; kwakuwa ndani yake kuna malipo na fadhila kubwa.
  • Starehe za dunia ni ndogo na matamanio yake ni yenye kuondoka.

Soma kwenye HadeethEnc.com

5 mara 100

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

Maana na chanzo

Imepokelewa Kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake-yakwamba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Atakayesema: Sub-haanallahi wabihamdihi, (Ametakasika Mwenyezi Mungu na sifa njema ni zake) kwa siku mara mia moja (100), yatafutwa madhambi yake hata kama yatakuwa na wingi mfano wa povu la Bahari".

Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake Daraja: Sahihi

Maelezo

Anaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa atakayesema kwa siku mara mia moja (100): "Sub-haanallaahi Wabihamdihi"; Yatafutwa makosa yake na yatasamehewa, hata kama yatakuwa mengi mfano wa taka nyeupe (povu) zinazoelea Baharini wakati mawimbi yanapotembea na yanapopiga.

Faida

  • Malipo haya anayapata atakayelisema neno hilo ndani ya siku nzima mfululizo au kwa nyakati tofauti tofauti.
  • Tasbihi: Ni kumtakasa Allah kutokana na mapungufu, na kumhimidi: Ni kumsifu kwa ukamilifu pamoja na kumpenda na kumtukuza.
  • Makusudio katika hadithi hii ni kufutwa madhambi madogo madogo, ama madhambi makubwa haya ni lazima yafanyiwe toba.

Soma kwenye HadeethEnc.com

6 Mara moja

سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِحَمْدِهِ

Maana na chanzo

Imepokelewa kutoka kwa Jabiri -radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Atakayesema: Sub-haanallaahi wabihamdi, (Ametakasika Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa njema ni zake) ataoteshewa mti wa mtende peponi".

Imepokelewa Imamu Tirmidhiy Daraja: Sahihi

Maelezo

Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake yakuwa atakayesema: "Ametakasika Mwenyezi Mungu" ninamtakasa "Mtukufu" kwa dhati yake na sifa zake na vitendo vyake "na sifa njema ni zake" zikiwa zimeambatanishwa na kuegemeza sifa za ukamilifu wake Mtukufu; atasimikiwa na kupandiwa mti wa mtende katika ardhi ya Pepo kwa kila mara atakayosema.

Faida

  • Himizo la kukithirisha kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na miongoni mwake: Ni kufanya tasbihi na tahmidi (kumtukuza na kumsifu).
  • Pepo ni pana, na kwamba mimea yake ni tasbihi na tahmidi (Kumtuza na kumsifu), na hii ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na neema yake.
  • Umetajwa mtende pekee katika hadithi pasina miti mingine; kwa sababu ya wingi wa faida zake na uzuri wa matunda yake; na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu amepiga mfano wa muumini na imani yake ndani ya Qur'ani kwa mti huo.

Soma kwenye HadeethEnc.com

7 Mara moja

لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، اللهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا، سُبْحَانَ اللهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Sa'di radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Alikuja bedui kwa Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake akasema: Nifundishe maneno nitakayoyasema. Akasema "Sema: Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu yeye pekee asiyekuwa na mshirika, Mwenyezi Mungu mkubwa mno, na kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu kwa wingi, na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu, na hapana ujanja wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu mwenye nguvu na hekima" Akasema: Haya ni kwa ajili ya Mola wangu, yako wapi ya kwangu? Akasema: "Sema: "Ewe Mwenyezi Mungu nisamehe mimi na unihurumie na uniongoze na uniruzuku".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Mtu mmoja miongoni mwa watu wa kijijini alimuomba Mtume rehema na amani ziwe juu yake amfundishe dhikiri atakayokuwa akiisema, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Sema: "Laa ilaaha illa llaah wahdahu laa shariika lahu" (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika wake) Ameanza kwa shahada ya tauhidi, na maana yake hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, "Allaahu Akbaru kabiira" Yaani: Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko kila kitu na ni Mtukufu, "Na Alhamdulillaahi kathira" Yaani: Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu kwa wingi, kwa sifa zake na vitendo vyake na neema zake zisizohesabika, "Sub-haanallaahi rabbil Aalamiin" Yaani: Ametukuka na kutakasika na kila mapungufu, "Laa haulaa walaa quwwata illaa billaahil Azizil Hakiim" Yaani: Hakuna namna ya kugeuka kutoka hali moja kwenda hali nyingine isipokuwa kwa uweza wa Allah na msaada wake na taufiki yake, Yule bwana akasema: Maneno haya ni kwa ajili ya Mola wangu Mlezi, kwa kumtaja yeye na kumtukuza, ya kwangu mimi ya kujiombea mwenyewe yako wapi? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akasema kumwambia: Sema: "Ewe Mola wangu nisamehe" Kwa kuyafuta madhambi na kuyasitiri, "Na unihurumie" Kwa kuniletea manufaa na masilahi ya dini na dunia kwangu, "Na uniongoze" Kwenda katika hali nzuri na katika njia iliyonyooka, "Na uniruzuku" Mali ya halali na siha na kila aina ya kheri na afya.

Faida

  • Kuna himizo la kumtaja Mwenyezi Mungu kwa neno 'Laa ilaaha illa llaah, na Allaahu Akbar, na Alhamdulillaah, na Sub-haanallaah.
  • Ni sunna kumtaja Mwenyezi Mungu na kumsifu kabla ya kumuomba.
  • Ni suuna mtu kuomba kwa dua nzuri, na kwa dua zilizopokelewa toka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, ambazo zimekusanya kila aina ya kheri za Dunia na Akhera, na ana uhuru wa kuomba akitakacho.
  • Inampasa mja apupie kujifunza yale yenye kumnufaisha katika Dunia na Akhera.
  • Himizo la kuomba msamaha na huruma na riziki, kwani mambo haya yamekusanya kheri zote.
  • Huruma yake rehema na amani ziwe juu yake katika kuufundisha umma wake yale yenye kuwanufaisha.
  • Imetajwa huruma baada ya msamaha ili usafi ukamilike,na msamaha ni kusitiriwa makosa na kufutwa kwake na kuepushwa na moto, na huruma ni kufikishiwa kheri na kuingia peponi, na huku ndiko kufaulu kukubwa.

Soma kwenye HadeethEnc.com

8 Mara moja

رَضِيتُ بِاللَّهِ رَبَّاً، وَبِالْإِسْلَامِ دِيناً، وَبِمُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَبِيّاً

Maana na chanzo

Kutoka kwa Abuu Saidi Al-Khudri radhi za Allah ziwe juu yake, yakwamba Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Atakayesema nimeridhia Mwenyezi Mungu kuwa Mola, na kuwa Uislamu ni dini, na Muhammadi kuwa Mtume, basi atastahiki kwake Papo".

Imepokelewa na Abu Daud Daraja: Sahihi

Maelezo

Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa atakayesema: "Nimemridhia Mwenyezi Mungu kuwa Mola" na Mungu na Mlezi na Mmiliki, na bwana na Mtengenezaji, "na Uislamu" kwa hukumu zake zote kwanzia amri zake na makatazo yake "kuwa Dini" mila na sheria, itikadi na utii, "na Muhammadi kuwa Mtume" na Nabii; kwa yote aliyotumwa kwayo na akatufikishia, isipokuwa itamstahikia kwake Pepo.

Faida

  • Himizo la kusema dua hii, na kumebainishwa thawabu zinazoambatana nayo.
  • Kumridhia Mwenyezi Mungu kuwa Mola, kunaambatana na mtu kutomuabudu asiyekuwa yeye Mtukufu.
  • Kumridhia Muhammadi rehema na amani ziwe juu yake kuwa Nabii na Mtume, kunaambatana na kumtii rehema na amani ziwe juu yake na kutii sunna zake.
  • Kuridhia Uislamu kuwa dini ni kuridhia yale aliyoyachagua Mwenyezi Mungu kwa waja wake.
  • Sunna ya kusema dua hii wakati wa shahada mbili baada kusikia Adhana, kama ilivyokuja katika riwaya zingine.
  • Na imekuja katika hadithi nyingine sunna ya kuomba dua hii wakati wa asubuhi na jioni.

Soma kwenye HadeethEnc.com

9 Mara moja

Maana na chanzo

Imepokelea kutoka kwa Abii Maalik Al-Ash-ariy Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe ju yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani ziwe juu yake: "Twahara ni nusu ya imani, na kusema Al-hamdulillah neno hilo hujaza mizani, na neno Sub-hanallah neno Alhamdulillah maneno hayo mawili hujaza mizani- au hujaza- sehemu iliyopo kati ya Mbingu na Ardhi na Swala ni nuru, na sadaka ni dalili ya imani, na subira ni mwangaza, na Qur'ani ni hoja kwako au hoja dhidi yako, watu wote huamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kutafuta riziki kuna mwenye kuwa na msimamo na kumtii Mwenyezi Mungu, na akawa ni mwenye kuikomboa nafsi yake kutoingia motoni, na miongoni mwao kuna mwenye kuangukia kwenye maasi na akaangamia na kuingia motoni".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Anafahamisha Mtume Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa twahara na usafi wa nje ambao ni udhu na kuoga ni sharti la usahihi wa swala. Na kuwa neno: "Alhamdulillah hujaza mizani" nako ni kumsifu Mwenyezi Mungu aliyetakasika na machafu, na kumsifia kwa sifa za ukamilifu zitakazopimwa siku ya kiyama na kuijaza mizani ya matendo. Na kuwa neno: "Sub-hanallah na Alhamdulillah" na maneno hayo ni kumtakasa Mwenyezi Mungu na kumsifia kwa sifa zilizokamilika na zilizotimia ambazo anastahiki sifa hizo pamoja kumpenda yeye na kumtukuza hujaza sehemu iliyopo kati ya Mbingu na Ardhi. Na kuwa "Swala ni nuru" ya mja katika moyo wake, na katika uso wake na kaburini mwake na siku ya kufufuliwa kwake. Na kuwa "Sadaka ni ushahidi" Na ni dalili ya ukweli wa imani ya muumini, na tofauti yake na mnafiki ambaye huzuia kutoa sadaka kwa kuwa mnafiki haamini malipo ya kutoa sadaka. Na "kuwa subira ni mwangaza" -na subira ni kuizuia nafsi kutoku papatika na kuwa na hasira, subira ni nuru inayokuwa na joto na kuunguza, kama vile mwanga wa Jua; kwa sababu subira ni tabu kubwa inahitaji kuilazimisha nafsi na kuizuia na kile inachokipenda; hivyo haachi kuwa na mng'ao mtu mwenye subira, mwenye kuongoka na mwenye kudumu katika usahihi, nako ni kusubiri katika kumtii Mwenyezi Mungu, na kutomuasi yeye, na kuwa na subira kwenye matatizo na aina mbalimbali za mambo yenye kuchukiza katika Dunia. Na kuwa "Qur'ani ni hoja kwako wewe" kwa kuisoma na kuifanyia kazi, au yaweza kuwa " Hoja dhidi yako" kwa kuiacha pasina kuifanyia kazi au kuisoma. Kisha akafahamisha Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- yakuwa watu wote huenda mbio na hutawanyika na huamka toka usingizini mwao na wanatoka kwenye majumba yao kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali miongoni mwao kuna wenyekuwa na msimamo katika kumtii Mwenyezi Mungu, hivyo anakuwa ameikomboa nafsi yake na moto, na miongoni mwao kuna mwenye kwenda kinyume na kuacha kumtii Mwenyezi Mungu na akaingia katika maasi, hivyo akaiangamiza na kuingia motoni.

Faida

  • Twahara zipo aina mbili: Twahara ya nje nayo ni udhu na kuoga, na twahara ya ndani inakuwa kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na matendo mazuri.
  • umuhimu wa kuzihifadhi swala tano, kwakuwa swala tano ni mwangaza kwa mja hapa Duniani na siku ya Kiyama.
  • Kutoa sadaka ni dalili ya imani ya kweli.
  • Umuhimu wa kuifanyia kazi Qur'ani na kuisadikisha ili iwe ni hoja kwako au dhidi yako.
  • Ikiwa nafsi hutoishughulisha na utiifu itakushughulisha na maasi.
  • Kila mwanadamu lazima afanye matendo, hivyo ima aikomboe nafsi yake kwa kutii, au aiangamize kwa kufanya maasi.
  • Na subira inahitaji uvumilivu na kutarajia thawabu, na ndani yake kuna uzito.

Soma kwenye HadeethEnc.com

10 Mara moja

Maana na chanzo

Kutoka kwa bin Mas'udi radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake-: "Nilikutana na Ibrahimu usiku niliochukuliwa, Akasema: Ewe Muhammadi wafikishie umma wako salamu zangu, na uwaeleze kuwa pepo ina udongo mzuri, ina maji matam, nakuwa imenyooka na kulingana sawa, nakuwa mimea yake: ni (kusema) Sub-haana llaah -Ametakasika Mwenyezi Mungu, Na Alhamdulillaah -Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu, Na Laa ilaaha illa llaah -Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Allaahu Akbar -Mwenyezi Mungu Mkubwa".

Imepokelewa Imamu Tirmidhiy Daraja: Ni Nzuri kwa Ushahidi wake mbalimbali

Maelezo

Anaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa alikutana na Ibrahim mwandani amani iwe juu yake usiku aliposafirishwa kwenda mbinguni (Israa wal Miiraji), akasema kumwambia: Ewe Muhammadi: Wafikishie umma wako kutoka kwangu salamu, na ulijulishe kuwa Pepo ina udongo mzuri, ina maji matam yasiyokuwa na chumvi, na kuwa Pepo ni pana, ni tambarare haina miti, na kuipanda kwake ni kwa maneno mazuri, nayo ni mema yenye kubakia: Sub-haanallaah, Alhamdulillaah, wa Laa ilaaha illa llaah, wallaahu Akbaru, kila anapoyasema muislamu na kuyarudiarudia hupandia mmea Peponi.

Faida

  • Himizo la kudumu na dhikiri ili kukithirisha mimea ya Pepo.
  • Fadhila za umma wa kiislamu; kiasi kwamba Ibrahim amani iwe juu yake aliutumia salam.
  • Himizo la Nabii Ibrahim amani iwe juu yake kwa umma wa Muhammad rehema na amani ziwe juu yake la kukithirisha kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu.
  • Amesema Attwayibi: Pepo ni uwanda (tambarare), kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa fadhila zake akaweka ndani yake miti na magorofa kulingana na matendo ya watendaji; kila mfanyaji atakuwa na nafasi maalum kwa sababu ya matendo yake, kisha Mwenyezi Mungu alipompa wepesi wa kufanya matendo aliyoumbiwa ili azipate thawabu hizo, akamfanye yeye kuwa ni kama mpandaji wa miti hiyo.

Soma kwenye HadeethEnc.com

11 Mara moja

Maana na chanzo

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Hawajawahi kukaa watu kikao chochote wakawa hawakumtaja Mwenyezi Mungu ndani yake, na wala hawakumsalia Nabii wao, isipokuwa itakuwa ni hasara juu yao, akitaka atawaadhibu na akitaka atawasamehe".

ImepokAbu Daud, Tirmidhiy na Nasai katika kitabu Alkubraa Daraja: Sahihi

Maelezo

Ametahadharisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake kughafilika kumtaja Mwenyezi Mungu, nakuwa hawatokaa watu katika kikao chochote na wakawa hawakumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake, na wakawa hawakumsalia Mtume wake rehema na amani ziwe juu yake isipokuwa kikao hicho kitakuwa ni hasara na majuto juu yao na mapungufu siku ya Kiyama, akitaka atawaadhibu kwa madhambi yao yaliyotangulia na uzembe wao uliofuata, na akitaka atawasamehe ikiwa ni fadhila na rehema kutoka kwake.

Faida

  • Himizo la kufanya dhikiri na fadhila zake.
  • Fadhila za vikao ambavyo anatajwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake, na kumtaja Mtume wake rehema na amani ziwe juu yake, nakwamba vikao ambavyo havina hayo ni vikao vibaya kwa watu siku ya Kiyama.
  • Tahadhari iliyotajwa ya kughafilika kumtaja Mwenyezi Mungu haishii katika vikao pekee, bali inaenea katika sehemu zingine, amesema Nawawi: Ni machukizo kwa atakayekaa mahali aondoke bila kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani yake.
  • Masikitiko yatakayotokea siku ya Kiyama: Ima ni kwa sababu ya kupoteza malipo na thawabu kwa kutofaidika na wakati kwa kumtii Mwenyezi Mungu, na ima ni kwa madhambi na adhabu kwa kuutumia wakati kwa kumuasi Mwenyezi Mungu.
  • Tahadhari hii ni pale kughafilika kutakapokuwa ni kwa mambo ya halali, je, ni vipi vikiwa vikao vya haramu ambavyo ndani yake kuna utesi na usengenyaji na mengineyo?!.

Soma kwenye HadeethEnc.com

Maswali

Kuna nini kwenye ukurasa huu?

Dhikri bora zaidi: kila moja kwa Kiarabu, pamoja na maana yake, hadithi inakotoka, daraja yake na maelezo.

Tafsiri zinatoka wapi?

Kutoka HadeethEnc.com, Ensaiklopidia ya Hadithi za Mtume Zilizotafsiriwa. Kila hadithi inaonyeshwa kama walivyoichapisha, pamoja na chanzo na daraja yake, na viungo vya asili.

Kihesabu kinafanyaje kazi?

Gusa kihesabu chini ya dhikri na kitahesabu kurudi nyuma hadi sifuri. Kipo kwenye ukurasa huu tu na hakuna kinachohifadhiwa.

Naweza kupata kikumbusho cha kila siku?

Ndiyo. Programu ya bure ya Qabas kwa Android inakukumbusha adhkar za asubuhi na jioni kila siku na ina kihesabu hicho hicho.