Adhkar baada ya swala (baada ya kila swala)

Utajo wa Allah unaosemwa baada ya swala za faradhi, baada ya kutoa salamu.

1 Mara moja

أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ (٣)، اللَّهُمَّ أَنْتَ السَّلَامُ وَمِنْكَ السَّلَامُ، تَبَارَكْتَ يَا ذَا الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Thauban -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- anapoondoka katika swala yake anaomba msamaha mara tatu, na anasema: "Allaahumma antas salaam waminkas salaam, tabaarakta yaa dhal-jalaali wal-ikraam", Anasema Walid: Nikasema kumwambia Auzaiy: Ni vipi unaomba msamaha: Akasema: Unasema: Astagh-firullaah, Astagh-firullaah.

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema anapomaliza swala yake: Astagh-firullaah, Astagh-firullaah, Astagh-firullaah.

Kisha anamtukuza Mola wake Mlezi kwa kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe ni amani, na amani inatoka kwako, umetukuka ewe mwenye utukufu na ukarimu" Mwenyezi Mungu aliyesalimika na kukamilika katika sifa zake, aliyetakasika na kila aibu na mapungufu, na unaomba kutoka kwake Mtukufu amani kutokana na shari za dunia na akhera na si kwa mwingine asiyekuwa yeye, naye Mtukufu kheri zake ni nyingi duniani na akhera, mwenye utukufu na wema na ihisani.

Faida

  • Sunna ya kuomba msamaha baada ya swala na kudumu nazo.
  • Sunna ya kuomba msamaha ili kuziba mapungufu ndani ya ibada na kuipa nguvu ibada na uzembe uliojitokeza ndani yake.

Soma kwenye HadeethEnc.com

2 Mara moja

لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Warraadi mwandishi wa Mughira amesema: Alinisomea Mughira bin Shu'ba katika kitabu kilichoandikwa kwenda kwa Muawia: Yakwamba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- alikua akisema mwishoni mwa kila swala ya faradhi: "Laa ilaaha illa llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul mulku walahul hamdu, wahuwa a'laa kulli shai in qadiir, Allaahumma laa maania limaa a'twaita walaa mu'twiya limaa mana'ta, walaa yanfa'u dhal jaddi minkal jaddu".

Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake Daraja: Sahihi

Maelezo

Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema kabla kidogo ya mwisho wa kila swala ya faradhi: "Laa ilaaha illa llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul mulku walahul hamdu, wahuwa a'laa kulli shai in qadiir, Allaahumma laa maania limaa a'twaita walaa mu'twiya limaa mana'ta, walaa yanfa'u dhal jaddi minkal jaddu"

Yaani: Nina kiri na kulikubali neno la kumpwekesha Allah, la Laa ilaaha illa llaah, -Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah-, ibada ya kweli naithibitisha kwa Mwenyezi Mungu, na ninaikanusha kwa asiyekuwa yeye, hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allah, na ninakiri kuwa ufalme wa kweli uliotimia ni wa Mwenyezi Mungu, na sifa zote za viumbe wa mbinguni na ardhini zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, kiasi kwamba yeye ndiye muweza juu ya kila kitu, na aliyoyakadiria Mwenyezi Mungu katika vipawa au kunyimwa hakuna awezaye kuyazuia, na hapo basi utajiri hauwezi kumsaidia mwenye nao, bali kinachoweza kumfaa ni amali zake.

Faida

  • Kupendeza kusomwa dua hii mwisho wa swala kwakuwa imekusanya lafudhi za tauhidi na himdi.
  • Kufanya haraka kuitekeleza sunna, na kuitangaza.

Soma kwenye HadeethEnc.com

3 Mara moja

لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللهِ، لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، ‌وَلَا ‌نَعْبُدُ ‌إِلَّا إِيَّاهُ، لَهُ النِّعْمَةُ وَلَهُ الْفَضْلُ وَلَهُ الثَّنَاءُ الْحَسَنُ، لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Abuu Zubairi amesema: Alikuwa bin Zubairi akisema mwisho wa kila swala anapotoa salamu: "Laa ilaaha illa llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul Mulku walahul-hamdu wahuwa a'laa kulli shai-in qadiir, Laa haula walaa quwwata illaa billaah, Laa ilaaha illa llaah, walaa na'budu illaa iyyaahu, Lahun-ni'matu walahul-fadhlu walahuth-thanaaul hasan, Laa ilaaha illa llaahu Mukhliswiina lahud-diina walau karihal kaafiruun" Na akasema: "Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akitoa tahlil (Laa ilaaha illa llaah) kwa maneno haya mwisho wa kila swala".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akinyanyua sauti baada ya salamu ya kila swala ya faradhi kwa dhikri hii tukufu, na maana yake:

"Laa ilaaha illa llaahu": Yaani: Hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.

"Wah-dahu Laa shariika lahu" Yaani: Hana ushirika katika Uungu wake na Uumbaji wake na Majina yake na Sifa zake.

"Lahul Mulku" Yaani: Ana Ufalme usio na mipaka mpana na ulioenea kila kitu, Ufalme wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo.

"Walahul-hamdu" Yaani: Yeye ndiye anasifika kwa ukamilifu usio na kikomo, mwenye kusifika kwa ukamilifu na kwa kupendwa na kutukuzwa kwa hali zote, katika furaha na majonzi.

"Wahuwa alaa kulli shai-in qadiir": Uwezo wake umekamilika na umetimia kwa namna zote, hakimshindi kitu, na hakuna jambo lolote linalokataa katika mambo yote.

"Laa haulaa walaa quwwata illa billaah" Yaani: Hakuna kugeuka kutoka hali moja kwenda nyingine, na kutoka katika kumuasi Mwenyezi Mungu kuja katika kumtii, na hakuna nguvu ila ni kwa Mwenyezi Mungu Yeye ndiye msaidizi na kwake ndiko kwa kutegemewa.

"Laa ilaaha illa llaah, walaa na'budu illa iyyaah": (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na hatumuabudu yeyote ila Yeye) Huu ni msisitizo wa maana ya Uungu na kukemea shirki, nakuwa hakuna anayestahiki kuabuduiwa zaidi yake.

"Lahun-ni'matu wal fadhlu: (Ni mmiliki wa neema na fadhila) Yeye ndiye anaumba neema na kuzimiliki, na humfadhilisha amtakaye katika waja wake.

"Walahuth thanaaul hasan" (Na ni zake sifa nzuri): Juu ya dhati yake na sifa zake na matendo yake na neema zake, na kwa kila hali.

"Laa ilaaha illa llahu, Mukhliswiina lahud-diin: Hapana Mola mwingine isipokuwa Yeye, tunamtakasia Yeye matendo yote: Yaani: Tunampwekesha si kwa kutaka kujionyesha wala kutaka kusikika katika kumtii Mwenyezi Mungu.

"Walau karihal kaafiruun", (Hata kama makafiri watachukia) Yaani: Tumethubutu katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu na ibada zake hata kama makafiri watachukia.

Faida

  • Sunna ya kudumu na adhkari za baada ya swala za faradhi.
  • Muislamu hujifaharisha kwa dini yake, na hudhihirisha nembo zake, hata kama makafiri watachukia.
  • Linapokuja katika hadithi neno: "Mwisho wa swala", Ikiwa kilichotajwa ndani ya hadithi ni dhikri, basi asili yake hapa ni baada ya salamu, na ikiwa ni dua inakuwa kabla ya salamu ndani ya swala.

Soma kwenye HadeethEnc.com

4 Mara moja

سُبْحَانَ اللَّهِ (٣٣)، الْحَمْدُ لِلَّهِ (٣٣)، اللَّهُ أَكْبَرُ (٣٣)، لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Maana na chanzo

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -Allah amridhie- kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakaye msabihi Mwenyezi Mungu mwisho wa kila swala mara thelathini na tatu (33), na akamhimidi Mwenyezi Mungu mara thelathini na tatu (33), na akamtukuza Mwenyezi Mungu mara thelathini na tatu, hizo ni tisini na tisa (99) Na akasema ili kukamilisha mia moja (100): Laa ilaaha illa llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul Mulku walahul hamdu, wahuwaa'laa kulli shai in qadiir, basi yatasamehewa madhambi yake, hata kama yalikuwa na wingi mfano wa povu la Bahari".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Anaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa atakayesema baada ya kumalizika kwa swala za faradhi:

Mara thelathini na tatu (33): (Sub-haanallaah) Nako ni kumtakasa Mwenyezi Mungu dhidi ya mapungufu.

Na mara thelathini na tatu (33): (Alhamdulillaah) Nako ni kumsifu Mwenyezi Mungu kwa sifa kamilifu pamoja na kumpenda na kumtukuza.

Na mara thelathini na tatu (33): (Allaahu Akbar) Nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkuu na Mtukufu kuliko kila kitu.

Na kwa kukamilisha idadi ya mia moja (100) "Laa ilaaha illa llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul Mulku, walahul hamdu, wahuwa alaa kulli shai in-Qadiir" Na maana yake: Hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, Yeye pekee asiye na mshirika, nakuwa Yeye Mtukufu ndiye alipwekeka kwa Ufalme kamilifu, na ndiye mwenye kustahiki kutukuzwa na sifa pamoja na mapenzi na kukwezwa pasina mwingine, nakuwa Yeye ni muweza hakuna kinachomshinda.

Yeyote atakayesema hivyo, dhambi zake zitafutwa na kusamehewa, hata zikiwa nyingi, kama povu jeupe litokalo juu ya bahari inapochafuka na kutibuka.

Faida

  • Sunna ya dhikiri hizi kuzisema baada ya swala za faradhi.
  • Dhikiri hizi ni sababu ya kusamehewa madhambi.
  • Ukubwa wa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu na rehema zake na msamaha wake.
  • Dhikiri hii ni sababu ya kusamehewa madhambi, na kinachokusudiwa hapa ni: kufutiwa madhambi madogo, ama madhambi makubwa hakuna kinachoweza kuyafuta isipokuwa toba.

Soma kwenye HadeethEnc.com

5 Mara moja

Maana na chanzo

Kutoka kwa Ka'b Bin Ujrah Radhi za Allah ziwe juu yake kutoka kwa Mtume rehema na amani za Allah ziwe juu yake alisema: "Adh-kari za baada ya sala ya faradhi hapati hasara msomaji au mfanyaji wake, kusema Sub-haana llahi mara thelathini na tatu (33), Al-hamdulillahi mara thelethini na tatu (33), Allahu Akbaru mara thelathini na nne (34)".

Imepokelewa Imamu Muslim Daraja: Sahihi

Maelezo

Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu Adhkari (Dua) hatopata hasara wala kujuta msemaji wake, bali maneno haya yanathawabu, na yanakuja kwa kufuatana, na husemwa baada ya swala za faradhi, nayo ni:

"Sub-haana llaah" -Ametakasika Mwenyezi Mungu- mara thelathini na tatu, yaani ametakasika Mtukufu na kila mapungufu.

"Na Alhamdulillaah" Mara thelathini na tatu, nako ni kumsifu Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu uliotimia pamoja na kumpenda na kumtukuza.

"Allaahu Akbaru" Mara thelathini na nne, Mwenyezi Mungu ni mkubwa mno na ni Mtukufu na Mwenye nguvu kuliko kila kitu.

Faida

  • Fadhila za kusema Sub-haanallaah, na Alhamdulillaah, na Allaahu Akbar, maneno haya ndio mema yenye kubakia.

Soma kwenye HadeethEnc.com

6 Mara moja

اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مَنْ ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Abuu Umama -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Yeyote atakayesoma Ayatul Kursiy mwisho wa kila swala ya faradhi hakuna kitakachomzuia kuingia peponi isipokuwa kufa".

Imepokelewa na Nasai katika kitabu Alkubraa Daraja: Sahihi

Maelezo

Mtume rehema na amani ziwe juu yake amesema kuwa mwenye kusoma Ayatul-Kursi baada ya kumalizika kwa swala ya faradhi, hakuna kitakachomzuia kuingia Peponi isipokuwa kifo; nayo iko katika Suratul Baqarah, Mwenyezi Mungu anasema: "Mwenyezi Mungu - hapana mungu isipokuwa Yeye, Aliye hai, Msimamizi wa mambo yote milele. Hashikwi na kusinzia wala kulala. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake isipokuwa kwa idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao, wala wao hawajui vyema chochote katika elimu yake isipokuwa kwa kile akitakacho. Kuti chake cha enzi kimeenea mbingu na dunia, na wala halemewi na kuvilinda vyote viwili. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu." [Al-Baqara: 255]

Faida

  • Fadhila ya Aya hii tukufu; kwa kukusanya kwake majina mazuri, na sifa za hali ya juu.
  • Sunna ya kusoma Aya hiyo tukufu baada ya swala za faradhi.
  • Matendo mema ni sababu ya kuingia peponi.

Soma kwenye HadeethEnc.com

7 Mara moja

اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ، وَشُكْرِكَ، وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

Maana na chanzo

Kutoka kwa Muadhi bin Jabali -radhi za Allah ziwe juu yake-: Yakwamba Mtume rehema na amani ziwe juu yake alimshika mkono wake, na akasema: "Ewe Muadhi, Wallahi hakika mimi ninakupenda", Akasema: "Ninakuusia ewe Muadhi usijekuacha mwisho wa kila swala kusema: Allaahumma ainni alaa dhikrika washukrika wahusni ibaadatika" Ewe Mwenyezi Mungu nisadie katika kukutaja na kukushukuru na kuzifanya vizuri ibada zako".

Imepokelewa na Abu Daud, Nasai na Ahmad Daraja: Sahihi

Maelezo

Mtume rehema na amani ziwe juu yake alishika mkono wa Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake, na akasema kumwambia: Wallahi hakika mimi ninakupenda, na ninakuusia ewe Muadhi usijekuacha kusema mwisho wa kila swala: Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie kukutaja, katika kila kauli na kitendo kinachoniweka karibu na utiifu, "na kukushukuru" kwa kutimia neema na kuzuia mabaya, "na kuzifanya vizuri ibada zako" kwa kutakasa nia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa kumfuata Mtume rehema na amani ziwe juu yake.

Faida

  • Sheria ya kumueleza mtu kuwa unampenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
  • Inapendeza kuomba dua hii mwisho wa kila swala ya faradhi na ya sunna.
  • Katika kuomba kwa matamshi haya machache kuna mahitaji yote ya Dunia na Akhera
  • Katika faida za kupendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni kuusiana katika na kupeana nasaha katika mambo mema na uchamungu.
  • Amesema Attwayibi: Kumtaja Mwenyezi Mungu ni utangulizi wa kukunjua kifua, na kumshukuru ni njia ya kuzilinda neema, na kuzifanya vizuri ibada ni kujiweka mbali na yote yanayomshughulisha mtu na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Soma kwenye HadeethEnc.com

Maswali

Kuna nini kwenye ukurasa huu?

Adhkar baada ya swala: kila moja kwa Kiarabu, pamoja na maana yake, hadithi inakotoka, daraja yake na maelezo.

Tafsiri zinatoka wapi?

Kutoka HadeethEnc.com, Ensaiklopidia ya Hadithi za Mtume Zilizotafsiriwa. Kila hadithi inaonyeshwa kama walivyoichapisha, pamoja na chanzo na daraja yake, na viungo vya asili.

Naweza kupata kikumbusho cha kila siku?

Ndiyo. Programu ya bure ya Qabas kwa Android inakukumbusha adhkar za asubuhi na jioni kila siku na ina kihesabu hicho hicho.